Loading...
title : Programu ya Lipa Kulingana na Matokeo Imeleta Mageuzi Katika Sekta ya Elimu.
link : Programu ya Lipa Kulingana na Matokeo Imeleta Mageuzi Katika Sekta ya Elimu.
Programu ya Lipa Kulingana na Matokeo Imeleta Mageuzi Katika Sekta ya Elimu.
Na Ismail Ngayonga- Maelezo.
SEKTA ya Elimu ni miongoni mwa vipaumbele muhimu vya maendeleo vilivyopewa mkazo na Serikali ya Awamu ya Tano katika kufanikisha utoaji wa huduma muhimu kwa wananchi ili kuchochea adhma ya kufikia uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.
Kupitia Sera Mpya ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014, Serikali imeazimia kutekeleza mipango mbalimbali ikiwemo utoaji elimu ya msingi bila ada, kuongeza ubora wa elimu kwa kuimarisha ukaguzi shuleni, na kuboresha miundombinu.
Aidha Serikali ilikusudia pia kuhakikisha upatikanaji wa vifaa stahili vya kufundishia na kujifunzia, kuongeza ubora wa walimu kwa kutoa mafunzo, motisha pamoja na udhibiti wa taaluma ya ualimu.
Ili kufanikisha malengo hayo, Serikali imekuwa ikitekeleza miradi, mipango na programu mbalimbali za elimu ili kuleta maendeleo ya haraka ya rasilimali watu kwa kutayarisha idadi ya kutosha ya Watanzania walioelimika na kupenda kujielimisha.
Miongoni mwa Programu hizo ni Programu ya Lipa Kulingana na Matokeo inayotekelezwa na Serikali katika kipindi cha miaka mitano 2014-18 iliyokusudia kuimarisha usimamizi wa raslimali fedha na manunuzi ya umma katika mipango ya elimu kwa Serikali Kuu na Serikali za Mitaa.
Programu hiyo inatekelezwa katika sekta za elimu ya msingi na Sekondari na kufadhiliwa na Benki ya Dunia, Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Sweden (SIDA) na Ubalozi wa Uingereza
Aidha programu hiyo pia imelenga kuanzisha njia ya moja kwa moja ya ugharimiaji elimu inayolenga kuipa motisha Serikali katika utekelezaji wa mipango inayolenga matokeo ya haraka.
Maeneo muhimu yaliyochaguliwa kupitia programu hiyo ni pamoja na utoaji wa zawadi na motisha ya fedha na zisizo za fedha kwa walimu na shule zilizofanya vizuri, kutoa mafunzo kazini kwa walimu na kuimarisha mfumo wa Serikali na kufanya ufuatiliaji ya utolewaji na utumiaji wa fedha za ruzuku.
Aidha kupitia programu hiyo Serikali imekusudia kuimarisha uwazi wa matokeo ya mitihani kwa shule za Msingi na Sekondari na kufanya tathimni ya kujua kusoma, kuhesabu na kuandika kwa shule za halmashauri zilizoteuliwa katika zoezi hilo.
Katika kuhakikisha kuwa Programu hiyo inaleta tija iliyokusudiwa, Serikali imeanisha vipaumbele vikuu vitatu vinavyotumika katika kila Halmashauri ili kupima matokeo na kutoa motisha (fedha) kulingana na mahitaji na matumizi iliyojiwekea.
Vipaumbele hivyo ni pamoja na upangaji wa walimu katika shule zenye mahitaji, upelekaji wa ruzuku ya fedha za shule kutoka hazina pamoja na uwezo wa halmashauri kukusanya takwimu kwa usahihi na kuziweka mtandaoni kwa wakati.
Taarifa ya Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia inasema kuwa hadi sasa kiasi cha Tsh. Bilioni 90 zimeweza kupatikana kutokana na Serikali kutekeleza vipaumbele vyake kwa ufanisi kulingana na fedha za motisha zinazotolewa katika kila Halmashauri iliyopo katika mradi huo.
Aidha Serikali imetoa kiasi cha Tsh. Bilioni 22 za motisha kwa Halmashauri 179 zilizohakikiwa kwa mwaka 2015/16 ambapo zilitolewa kufuatana na viwango vya utekelezaji wa viashiria vya utendaji katika sekta ya elimu.
Akiwasilisha Hotuba ya makadirio ya Bajeti ya mwaka 2017/18, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI George Simbachawene anasema Programu ya Lipa kulingana na matokeo imekusudia kuongeza ufanisi na uwajibikaji wa kutoa elimu nchini na kujenga uwezo wa Serikali wa kutekeleza vipaumbele vyake ilivyojiwekea.
Anasema Programu hiyo imeweza kuongeza kiwango cha ufaulu wa Mtihani wa Taifa wa Darasa la Nne na Darasa la Saba, kutokana na jitihada zilizofanywa na Serikali katika kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia.
“Ufaulu katika Mtihani wa Taifa wa Kumaliza Shule ya Msingi umeongezeka kutoka asilimia 68.4 mwaka 2015 hadi asilimia 70.36 mwaka 2016. Wanafunzi wote waliofaulu Mtihani huo wamechaguliwa kujiunga na Kidato cha Kwanza mwaka 2017” anasema Simbachawene.
Aidha Simbachawene anasema kupitia Programu hiyo, Serikali katika mwaka 2016/17 imeweza kutoa mafunzo kwa Maafisa Elimu Vifaa na Takwimu 370 kutoka Halmashauri 184 na Maafisa Elimu Taaluma Mikoa 26 kuhusu matumizi ya mfumo wa uingizaji na utoaji wa takwimu kwa njia ya kielektroniki ili kuboresha upatikanaji wa takwimu za Elimu kwa usahihi na kwa wakati.
Kwa mujibu wa Simbachawene anasema Ofisi yake pia imeweza kusambaza nakala za vitabu 1,412,832 vya masomo ya Historia, Jiografia na Kiingereza kwa Kidato cha Kwanza hadi cha Nne na vitabu 159,737 vikiwemo 83,189 vya masomo ya sayansi na vitabu 76,548 vya masomo ya sanaa kwa Kidato cha Tano na Sita zilizopo katika Halmashauri 184 nchini.
Kuhusu ujenzi wa Maabara, Simbachawene anasema Serikali kupitia Mpango wa Uimarishaji wa Stadi za Kusoma Kuandika na Kuhesabu imefanikiwa kununua vifaa vya maabara vyenye thamani ya Tsh. bilioni 16 na kuvisambaza katika shule 1,696 zilizokamilisha ujenzi sawa na asilimia 47 ya shule za sekondari 3,602.
“Shule za Sekondari nchini zinahitaji maabara 10,840 na zilizopo kwa sasa ni 5,562 sawa na asilimia 51.3 na upungufu ni maabara 5,278 ambazo zinaendelea kujengwa” anasema Simbachawene.
Simbachawene anasema kupitia kupitia Mpango wa Elimu wa Lipa kwa Matokeo, Serikali kwa kushirikiana na SIDA, Ubalozi wa Uingereza na Benki ya Dunia imeweza kutumia kiasi cha Tsh. Bilioni 21 kwa ajili ya upanuzi wa miundombinu katika Shule 85 za Sekondari za Kidato cha Tano na Sita nchini.
Akifafanua zaidi Simbachawene anasema katika mwaka wa fedha 2016/17, Serikali imetuma kiasi cha Tsh. Bilioni 36.8 katika akaunti za Shule za Sekondari Kongwe 23 kwa ajili ya ukarabati na Tsh. Bilioni 3.5 zimepelekwa katika Shule saba (7) za Sekondari za Ufundi kwa ajili ya ukarabati wa karakana.
Dhana ya Programu ya Lipa kulingana na Matokeo ikieleweka kwa wadau wote na kufanyiwa kazi kulingana na viashiria vilivyowekwa itasaidia kuijengea Serikali utamaduni wa kufanya kazi kwa matokeo na kutekeleza malengo iliyojiwekea kwa wakati.
Aidha Programu hiyo itaisaidia Serikali kufikia azima na kusudio la kuboresha kiwango cha elimu itakayoleta ushindani na mchango mkubwa katika maendeleo ya viwanda nchini.
Hivyo makala Programu ya Lipa Kulingana na Matokeo Imeleta Mageuzi Katika Sekta ya Elimu.
yaani makala yote Programu ya Lipa Kulingana na Matokeo Imeleta Mageuzi Katika Sekta ya Elimu. Wakati huu, pengine unaweza kutoa faida na wewe wote. Sawa, kuona katika post nyingine makala.
Wewe ni sasa kusoma makala Programu ya Lipa Kulingana na Matokeo Imeleta Mageuzi Katika Sekta ya Elimu. mahali kiungo https://somalatest.blogspot.com/2017/06/programu-ya-lipa-kulingana-na-matokeo.html
0 Response to "Programu ya Lipa Kulingana na Matokeo Imeleta Mageuzi Katika Sekta ya Elimu."
Post a Comment