Loading...
title : RAIS JOSEPH KABILA: "MBONGO" ANAETAWALA WACONGOMANI DRC!!!
link : RAIS JOSEPH KABILA: "MBONGO" ANAETAWALA WACONGOMANI DRC!!!
RAIS JOSEPH KABILA: "MBONGO" ANAETAWALA WACONGOMANI DRC!!!
Rais JOSEPH KABILA ni raia wa Democratic Republic of Congo (DRC) lakini kwa kuwa amekulia Bongo kwa miaka mingi, basi ni dhahir shahir unaweza kumwita ni Mbongo! Ukweli huu unaakisiwa na usuli wa historia ya maisha yake.JOSEPH alizaliwa tarehe 4.6.1971 eneo la Hewabora kijijini Fizi, Kivu Kusini huko Mashariki mwa DRC ambapo alizaliwa pamoja na pacha wa kike aitwaye JAYNET.
JOSEPH alianza masomo ya shule ya msingi huko DRC lakini alikuja kuendelea na masomo yake jijini Dar Es Salaam, Tanzania mwaka 1977 baada ya baba yake, LAURENT DESIREE KABILA na mama yake, SIFA MAHANYA, kuhamia Tanzania baada ya miaka mingi ya kuishi msituni huko Kivu wakiendesha uasi dhidi ya Rais wa wakati huo, marehemu dikteta MOBUTU SESE SEKO KUKU NGBENGU WA ZABANGA.
Baada ya masomo ya shule ya msingi, JOSEPH alisoma masomo ya jioni ya taasisi ya Zanaki katika shule ya sekondari ya wasichana ya Zanaki. Akiwa Zanaki, alikuwa pia akipata mafunzo ya kareti toka kwa Sensei MASSAWE aliyekuwa "Karate Spurring Partner" wake. Akiwa kijana, JOSEPH alipewa jina la utani la "WAR BUS" kwani alipenda sana sinema za kivita na 'martial arts".
Miaka ya mwisho ya 1980s, JOSEPH alijiunga na Shule ya Sekondari ya Irambo ambako alisoma kidato cha tano na sita. Shule hiyo kuukuu iko jijini Mbeya ambayo sasa, kwa kumuenzi JOSEPH, imeweka kumbukumbu yake ambapo njia aliyokuwa akipita kwenda madarasani toka bwenini, imewekwa bango "JOSEPH KABILA ROAD". Aidha, bweni alimokuwa akilala sasa limegeuzwa na kuwa darasa "Form 11 B". Bw. SHAMBWEE SHITAMBALA, aliyekuwa CHADEMA na kisha kutimkia CCM na ambaye kwa sasa ni wakili wa kujitegemea jijini Mbeya, ni mmoja wa waalimu waliowahi kufundisha katika shule hiyo.
Baada ya kumaliza masomo yake ya kidato cha sita, JOSEPH alijiunga na mafunzo ya Jeshi la Kujinga Taifa. Mafunzo hayo ya lazima ya mwaka mmoja yalikuwa ni kwaajili ya kuwajengea uzalendo na ukakamavu vijana wa Kitanzania na yalianzishwa kwa mujibu wa "The National Service Act No. 16 of 1964 ('RE 2002)".
JOSEPH alijiunga na kambi ya KJ 834 MAKUTUPORA JKT "OPERESHENI VYAMA VINGI" 1992/93 ambapo alikuwa "D Coy" kwaajili ya mafunzo hayo. Kambini hapo, JOSEPH alikuwa ni kijana mkimya na mtaratibu. Alipenda sana mafunzo ya kijeshi na hakuwahi kujongo hata mara moja. Aidha, alipenda sana kupata habari mchanganyiko na alikuwa akitembea na kiredio chake kidogo mkononi na alikuwa msomaji mzuri wa "novel".
Hapa Dar Es Salaam, Mzee LAURENT DESIREE KABILA na familia yake waliishi eneo la Kunduchi Kilongawima karibu na bahari. Kwa kuogopa kubambwa na vikaragosi vya dikteta MOBUTU, mzee KABILA alikuwa akitumia jina feki la FRANCIS MTWALE au "Baba Cecy"(jina la mmoja wa watoto wake) na kudanganya kuwa yeye ni mfipa wa Sumbawanga!.
Mwanzoni, maisha ya familia hiyo yalikuwa ni ya kubangaiza na "kuungaunga" sana na hii ilipelekea watoto wa mzee huyo kusoma shule chovu. Mkewe, SIFA MAHANYA alilazimika kulima vimbogamboga na kwenda kuuza sokoni kwani walikuwa hoehae sana huku wakiwa na watoto wengi. Bi SIFA, baada ya mmewe kuwa Rais wa DRC, alikuja kuuelezea mwenyewe ufukara huo uliokuwa umetamalaki kwenye familia yao kwa muongo mingi ambapo tarehe 2.6.2006 alisema:
"If life in the bush in Kivu was difficult, in Tanzania it was much worse. We had nothing. I farmed a small field and sold my vegetables at the market like all poor African women".
Mzee KABILA akiwa nchini Tanzania alikuwa akizunguka nchi mbalimbali kutafuta 'support" ya kumng'oa MOBUTU. Hapo Kunduchi Kilongawima, familia hiyo ilipata nyumba ambayo ipo mpaka leo na panajulikana kama "Kwa KABILA". Akiwa Kilongawima, mzee huyo alikuwa maarufu kutokana na ucheshi na kupenda kujichanganya hasa na vijana. Alikuwa na Land Rover 104 yake nyeupe aliyokuwa akiitumia kubebea nyasi za ngombe alizokuwa akizichukua Mbuyuni njia ya Tegeta.
Baadhi ya watoto wa mzee KABILA wamezaliwa Dar As Salaam (ZOE(26.6.1979), CECYLIA na JOSEPHINE). Mmoja wa watoto wa Mzee KABILA aliyekuwa akipenda kwenda kupunga upepo baharini karibu na Kilongawima, alitokea kumpenda mvuvi mmoja mchovu Mzanzibar aliyekuwa akivua samaki mara kwa mara na wenzake katika eneo hilo. Baada ya maisha kuinyookea familia ya KABILA, mvuvi huyo kijana, baada ya kupata rizki mantashari hiyo toka kwa binti wa Mzee KABILA, kwa sasa ni milionea aliyeamua kurudi kwao Zanzibar anakomiliki moja ya kumbi kubwa za muziki Afrika Mashariki iliyoko kwenye eneo kubwa pembezoni ya Zanzibar. Mara kwa mara, "mvuvi" huyo hupenda kupiga stori maskani iliyopo jirani na ukumbi huo akiwa na washkaji zake ambapo ukimuona huwezi kuamini kuwa ndio "owner" kwani wengi wanadhani inamilikiwa na Muitaliano!.
JOSEPH alimaliza mafunzo ya JKT mwaka 1993. Kwa kuwa amekaa Tanzania kwa miaka yote hiyo, anakicharaza Kiswahili kama Mbongo tofauti na WACONGOMANI ambao wengi mara nyingi wanaongea Kifaransa na Kilingala huku lafudhi yao ya Kiswahili ikiwa na mushkeri.
Si Mzee KABILA pekee aliyekuwa akitumia jina feki alipokuwa Tanzania bali hata wanawe, kama alivyokuja kukiri mkewe SIFA baada ya kurejea DRC. Hata JOSEPH hakuwa akiitwa JOSEPH KABILA kama ilivyo sasa bali alijulikana kama JOSEPH KABANGE, lengo likiwa kutotumia jina "KABILA lililokuwa maarufu Zaire/DRC.
JOSEPH, baada ya mafunzo ya JKT, alienda Chuo Kikuu cha Makerere, Uganda.
Mzee KABILA, baada ya harakati za miongo mingi, hatimaye akafanikiwa, kwa msaada wa mataifa mbalimbali, kumng'oa dikteta MOBUTU na kuwa Rais wa tatu wa nchi hiyo tarehe 17.5. 1997.
Mwaka huohuo wa 1997 alimpeleka mwanae, JOSEPH, kwenda kwenye mafunzo ya kijeshi Beijing, China kwenye Chuo cha PLA National Defence University na aliporejea mwaka 1998, alimteua kuwa Meja Jenerali.
Mzee KABILA aliuawa tarehe 16.1.2001 baada ya "kutandikwa shaba" na mmoja wa walinzi wake ambapo aliacha watoto 25 aliozaa na wanawake 7. Idadi hii ilithibitisha alichokisema Rais DR. MAGUFULI tarehe 17.10.2016 pale Karimjee Hall wakati wa kutoa heshima za mwisho kwa aliyekuwa Meya wa zamani wa Dar Es Salaam, marehemu DIDAS MASABURI aliposema: "Ni jambo la kawaida kwa wanaume wa Kiafrika kuwa na wake wengi na watoto wengi. Hii idadi iliyotajwa hapa ya wake na watoto wake si sahihi, mi najua wapo wengi zaidi".
Tarehe 26.10.2001, JOSEPH akamrithi marehemu baba yake na kuwa Rais wa nne wa DRC. Akiwa amezaliwa mwaka 1971, JOSEPH alikuwa Rais wa kwanza duniani kuzaliwa miaka ya 1970s na kwa umri wake wa miaka 30, akawa ndiye Rais mdogo kuliko wote duniani!.
Tarehe 1.6.2006, Rais JOSEPH KABILA alimuoa Bi. OLIVE LEMBE DI SITA, ndoa iliyofungwa kanisani na kufuatiwa na harusi ya kukata na shoka ambapo watu walikula kunywa hadi majogoo!.
Rais JOSEPH KABILA na "First Lady" huyo wana watoto wawili ambapo mmoja ni wa kike aitwae SIFA, na mwingine ni wa kiume aitwaye LAURENT DESIREE (ambayo yote ni majina ya wazazi wa Rais JOSEPH KABILA).
Mwaka 2006, Rais JOSEPH KABILA alichaguliwa kuendelea kuwa Rais katika uchaguzi wa kwanza wa kidemokrasia toka nchi hiyo ipate uhuru toka kwa Ubelgiji mwaka 1960.
Rais JOSEPH KABILA alichaguliwa tena kuwa Rais mwaka 2011. Kwa kuwa Katiba ya DRC iliyopitishwa tarehe 18.2.2006 inampa Rais mihula miwili tu ya kutawala, mhula wake wa miaka mitano ya mwisho uliisha mwaka 2016 baada ya kucheleweshwa, uchaguzi umefanyika tarehe 30.12.2018 ambapo yeye hakugombea bali alipiga kura.
Tafakuri Tunduizi (Critical Thinking):
1. Je, iliwezekanaje Mcongoman JOSEPH kuhudhuria mafunzo ya JKT yaliyotolewa mahususi kwa vijana wa KITANZANIA?
2. Baada ya kuwatumikia wananchi wa DRC kama Rais, je "Mbongo" JOSEPH KABILA, atarejea Kunduchi Kilongawima alikokulia?
3. Je, uongozi wa Shule ya Sekondari ya Irambo ambayo imekuwa chovu una mikakati gani ya kuwatumia 'alumni wake hasa Mh JOSEPH KABILA ili kuikarabati?
4. Je, ni kwanini watoto wakizaliwa, mara nyingi, hupewa majina ya babu na bibi zao?
5. Je, ni sahihi kwa watoto wazaliwao kuchukua majina ya wazazi wa baba tu?
Tupia maoni yako.
Hivyo makala RAIS JOSEPH KABILA: "MBONGO" ANAETAWALA WACONGOMANI DRC!!!
yaani makala yote RAIS JOSEPH KABILA: "MBONGO" ANAETAWALA WACONGOMANI DRC!!! Wakati huu, pengine unaweza kutoa faida na wewe wote. Sawa, kuona katika post nyingine makala.
Wewe ni sasa kusoma makala RAIS JOSEPH KABILA: "MBONGO" ANAETAWALA WACONGOMANI DRC!!! mahali kiungo https://somalatest.blogspot.com/2019/01/rais-joseph-kabila-mbongo-anaetawala.html
0 Response to "RAIS JOSEPH KABILA: "MBONGO" ANAETAWALA WACONGOMANI DRC!!!"
Post a Comment