Loading...
title : Mauaji ya Pwani yafikia watu 12
link : Mauaji ya Pwani yafikia watu 12
Mauaji ya Pwani yafikia watu 12
*Polisi wanane, watuhumiwa ujambazi wanne wauawa
*Majambazi waonywa hakuna atakayenusurika
Mwandishi Wetu
MAUAJI yaliyotokea eneo la Jaribu Mpakani, wilaya ya Kibiti mkoani Pwani yamefikia watu 12, kati yao askari Polisi wanane na watuhumiwa wa ujambazi wanne.
Taarifa iliyotolewa jana na Kamishna wa Jeshi la Polisi, Operesheni na Mafunzo, Nsato Mssanzya, ilieleza kuwa watuhumiwa hao wa ujambazi waliuawa katika majibizano ya bunduki kati ya polisi na majambazi.
Kwa mujibu wa Mssanzya, askari waliouawa ni Inspecta Peter Kigugu; F.3451 CPL Francis; F.6990 PC Haruna; G.3247 PC Jackson; H.1872 PC Zacharia; H.5503 PC Siwale; H.7629 PC Maswi na H.7680 PC Ayoub.
Mauaji ya askari 8
Kamisha Mssanzya alisema kuwa mauaji ya askari hao yalifanyika juzi 12:15 jioni katika eneo la Mkengeni kijiji cha Uchembe kata ya Mjawa tarafa na wilaya ya Kibiti mkoani Pwani.
Alisema kundi la majambazi ambalo idadi yao bado haijafahamika wakiwa na silaha, walishambulia kwa risasi gari la Polisi aina ya Toyota Land Cruiser PT.3713 na kuua askari wanane.
Mbali na kuua askari hao, pia walimjeruhi askari namba F. 6456 PC Fredrick kwa kumpiga risasi ya mkono wa kushoto ambaye alipelekwa hospitali ya misheni Mchukwi kwa matibabu.
Yalivyofanyika
Taarifa zinaonesha kuwa kundi hilo la majambazi wakiwa na silaha walishambulia kwa risasi gari hilo la polisi na kuuwa askari wanane papo hapo.
Ilielezwa kuwa kabla ya kutokea mauaji hayo, gari hilo lilikuwa likitokea eneo la Jaribu Mpakani kwenye kizuizi cha barabara kwenda Bungu likiwa na askari hao walikuwa wametoka kubadilishana lindo.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, gari hilo lilipofika maeneo ya Mkengeni sehemu yenye mteremko na majani marefu, lilianza kushambuliwa na majambazi hao.
Ilielezwa kuwa majambazi hao walipiga risasi kwenye kioo cha mbele usawa wa dereva, hali iliyomsababishia dereva kupoteza uelekeo na gari kuingia kwenye mtaro wa barabara, ndipo majambazi hao wakafanya mauaji kwa askari hao.
Mauaji ya watuhumiwa 4
Kamisha Mssanzya katika taarifa yake alisema hatua za kiintelijensia na kiupelelezi zilichukuliwa juzi hiyo hiyo usiku na zikasaidia askari kufuatilia na kubaini maficho ya muda ya majambazi hao.
Taarifa hiyo ya Kamisha Mssanzya, ilieleza kuwa katika majibizano ya risasi kati ya askari Polisi na majambazi hao, ndipo watuhumiwa hao wanne waliuawa.
Hata hivyo, taarifa zingine kutoka vyanzo vyetu zilidai kuwa baada ya mauaji ya askari hao wanane, Polisi ilifanya mahojiano na watuhumiwa wa ujambazi waliokuwa wakishikiliwa mahabusu.
Mahojiano hayo kwa mujibu wa taarifa hizo, yalisaidia watuhumiwa kukubali kwenda kuonyesha eneo walikojificha wenzao, katika msitu wa kilima cha Mianzini, barabara ya Nyamisati kwenye majira ya nane usiku wa kuamkia jana.
Inadaiwa kuwa walipofika eneo hilo, watuhumiwa hao waliokuwa mbele kwenda kuonesha waliko wenzao, walishambuliwa na majambazi hayo kujeruhiwa na baadaye walikufa ndipo majibizano ya risasi yakaendelea baina yao na polisi.
Bunduki zilizopotea
Taarifa ambazo hazijathibitishwa Polisi, zilidai kuwa baada ya mauaji ya askari hao, majambazi hao walikimbia na silaha tisa kati ya hizo, SMG sita zikiwa na risasi 30 kila moja na Long range tatu.
Lakini taarifa ya Kamisha Mssanzya ilieleza kuwa baada ya majibizano ya risasi wakati watuhumiwa wanne wa ujambazi walipouawa, majambazi hao walitelekeza silaha nne; mbili zikiwa zilizoibwa wakati wa mauaji wa askari na mbili mali ya majambazi hao.
Msako wa moto
Akielezea kwa undani, Kamishna Mssanzya alisema tukio hilo ni baya na halikubaliki kwani hadi sasa Jeshi la Polisi limeshapoteza askari zaidi 10 katika matukio kama hayo.
Alisema wameshaanzisha operesheni maalumu ya moto na kutangaza kuwa hakutakuwa na msamaha, kwamba watatafutwa na kushughulikiwa na hakuna atakayenusurika.
Kamishna Mssanzya alisema mapambvano hayo hayana mwisho na kuonya kuwa katika operesheni hiyo, majambazi wataona sura halisi ya Jeshi la Polisi kwa kuwa dawa ya moto ni moto.
Alimaliza kwa kupiga marufuku pikipiki za biashara maarufu bodaboda kufanya kazi zaidi ya saa 12 jioni katika eneo lote la Mkuranga, Kibiti na Rufiji.
JPM aomboleza
Wakati huo huo, Rais John Magufuli jana alielezea kupokea kwa mshituko na masikitiko makubwa taarifa za vifo vya hao.
Taarifa ya Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu Gerson Msigwa, ilieleza kuwa
Rais Magufuli alimtumia salamu za rambirambi Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini IGP-Ernest Mangu, familia za askari wote waliouawa, Askari Polisi wote na Watanzania wote walioguswa na vifo hivyo.
“Nimeshtushwa na nimesikitishwa sana na vifo vya askari wetu wanane ambao wamepoteza maisha wakiwa wanalitumikia Taifa, naungana na familia za marehemu wote, Jeshi la Polisi na Watanzania wote katika kipindi hiki kigumu cha huzuni na majonzi ya kuondokewa na vijana wetu shupavu.
“Namuomba Mwenyezi Mungu atupe moyo wa subira, uvumilivu na ustahimilivu,” alisema Rais Magufuli katika taarifa hiyo.
Dk. Magufuli pia alilaani tukio hilo na matukio yote ya kuwashambulia askari Polisi wanaofanya kazi kubwa na muhimu ya kulinda raia na mali na kuwataka Watanzania wote watoe ushirikiano katika kukomesha vitendo hivyo.
ACT, CCM
Wakati huo huo, Chama Cha Mapinduzi jana kilituma salamu za pole kwa Mwenyekiti wa chama hicho, Rais Magufuli kutokana na mauaji hayo ya askari Polisi.
Taarifa ya CCm ilieleza kuwa salamu hizo ziliwasilishwa kwa Rais Magufuli na Katibu wa NEC Itikadi na Uenezi, Humphrey Polepole Ikulu jijini Dar es Salaam jana.
Akiwa ameambatana na Naibu Katibu Kuu CCM Tanzania Bara, Rodrick Mpogolo na Katibu wa Umoja wa Wanawake Tanzania, Amina Makilagi, Polepole alisema CCM imeshitushwa na tukio hilo na kutoa pole hizo.
Alisema askari hao wamekuwa wakifanya kazi katika mazingira magumu wakati wote kuhakikisha Watanzania wanakuwa salama pamoja na mali zao hivyo kuuwawa kwao ni jambo la kusikitisha.
Naye Katibu, Kamati ya Amani na Usalama wa chama cha ACT Wazalendo, Mohammed Babu, aliwataka Watanzania washikamane wakati huu wa majonzi ya kupoteza askari.
“Chama cha ACT Wazalendo kimepokea kwa masikitiko makubwa taarifa ya kushambuliwa na kuuawa kwa askari wanane wa Jeshi la Polisi jana jioni katika eneo la Jaribu Mpakani, wilayani Kibiti, mkoa wa Pwani.
“Chama cha ACT Wazalendo kinatoa pole kwa familia za mashujaa wetu hawa wanane waliouawa wakati wakilinda usalama wetu wananchi, Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Ernest Mangu pamoja na Jeshi zima la Polisi,” alisema.
Alisisitiza kuwa ACT Wazalendo wanaungana na kutoa mwito kwa Watanzania kushikamana na vyombo vya ulinzi na usalama katika kipindi hiki cha majonzi kwa Taifa pamoja na kutoa ushirikiano kwao kuhakikisha matendo ya namna hii yanakomeshwa.
Hivyo makala Mauaji ya Pwani yafikia watu 12
yaani makala yote Mauaji ya Pwani yafikia watu 12 Wakati huu, pengine unaweza kutoa faida na wewe wote. Sawa, kuona katika post nyingine makala.
Wewe ni sasa kusoma makala Mauaji ya Pwani yafikia watu 12 mahali kiungo https://somalatest.blogspot.com/2017/04/mauaji-ya-pwani-yafikia-watu-12.html
0 Response to "Mauaji ya Pwani yafikia watu 12"
Post a Comment