Loading...
title : MBARAKA MWINSHEHE UKOSEFU WA DAMU KUONGEZEWA KULISABABISHA KIFO CHAKE.
link : MBARAKA MWINSHEHE UKOSEFU WA DAMU KUONGEZEWA KULISABABISHA KIFO CHAKE.
MBARAKA MWINSHEHE UKOSEFU WA DAMU KUONGEZEWA KULISABABISHA KIFO CHAKE.
Na: Moshy Kiyungi,Tabora.
Kifo cha mwanamuziki Mbaraka Mwinshehe Mwaruka, kilisababishwa na ukosefu wa damu ya kumuongezea muda mfupi baada ya kupata ajali mjini Mombasa.
Ajali hiyo ilitokea Januari 12, 1979, wakati akipatiwa matibabu katika hospitali ya Makadara mjini Mombasa nchini Kenya.
MBARAKA MWINSHEHE ENZI ZA UHAI WAKE
Baadhi ya Watanzania kwa mapenzi yao makubwa, kila ifikapo Januari 12, kila mwaka, hufanya kumbukizi ya nguli huyo aliyeliletea sifa kubwa taifa letu kupitia muziki.
Mbaraka alikuwa nchini humo kwa ajili ya safari ya kikazi pamoja na kurekodi nyimbo zake wakati huo akiwa kiongozi wa bendi ya Super Volcano ya mjini Morogoro.
Wasifu wa nguli huyo unaeleza kuwa alizaliwa Juni 27, 1944 mjini Morogoro.
Mbaraka alikuwa na vipaji vingi vikiwemo vya kutunga na kuimba nyimbo ambazo zilikuwa zikiburudisha, zikielimisha na kutoa maonyo kwa jamii.
Mbaraka alikuwa bingwa wa kupiga gitaa la solo ambalo alilimudu hadi kufikia kuitwa ‘International Soloist’.Aidha aliweza kuongoza kwa ufanisi mkubwa bendi za Morogoro Jazz kwa bendi yake ya Super Volcano kwa miaka tofauti.
Mwinshehe alikuwa mtoto wa pili kuzaliwa kati ya watoto 12, kati yao ni yeye na wadogo zake Zanda na Matata ndio waliokuwa wanamuziki.Zanda alikuwa mwimbaji wa nyimbo za kizungu katika bendi ya Morogoro Jazz na Matata alikuwa akichanganya drums katika bendi hiyo hiyo.
Baba yake Mzee Mwinshehe Mwaruka alikuwa wa kabila la Waluguru, msomi aliyekuwa Karani katika mashamba ya Katani. Mama yake alikuwa wa kabila la Ngoni.
Kwa mujibu wa maelezo ya familia, babu yake Mbaraka alikuwa wa kabila la Wadoe kutoka Bagamoyo. Alipelekwa na Wakoloni kijiji cha Mzenga Kisarawe, mkoani Pwani akawe Chifu wa huko.
Baada ya kutawazwa kuwa Chifu, alioa wake tisa na kupata watoto zaidi ya 50 akiwemo baba yake Mbaraka, Mzee Mwaruka.
Tungo za nyimbo za Mbaraka zimejaa maudhui mema, ambazo zilimpandisha ‘chati’ hadi kuchaguliwa kuwa mmoja kati ya wasanii waliokwenda kuiwakilisha Tanzania katika mji wa Osaka nchini Japan mwaka 1970, ambako kulifanyika maonesho ya Biashara ya Kimataifa ya Expo70.
Tanzania iliwakilishwa na wasanii kadhaa akiwemo mzee Morris Nyunyusa, mlemavu wa macho, aliyekuwa na kipaji cha kupiga ngoma zaidi ya kumi kwa wakati mmoja.
Wengine walikuwa Wanasanaa toka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na kundi la Blass Band toka jeshi la Polisi lililokuwa likiongozwa na Mzee Mayagilo.
Aliporejea toka Japan, Mbaraka alitunga wimbo uitwao ‘Maonesho Japan’ akisimulia jinsi mafanikio makubwa yaliyopatikana katika maonesho hayo.
Kwa upande wa elimu Mbaraka Mwinshehe aliipata huko Kisarawe Middle School mwaka 1963.
Baadaye akaenda mjini Morogoro kuendelea na masomo. Mbaraka yaelezwa kwamba aliamua kuacha shule akiwa darasa la kumi ili awe mwanamuziki.
Kisa cha kuacha shule ilitokea siku moja mwaka 1965 wanamuziki wa Morogoro Jazz wakiwa wamepumzika nje ya Klabu yao, Mbaraka Mwinshehe alipita karibu yao akiwa kabeba begi kubwa. Walipomuuliza anaenda wapi muda ule ambao anatakiwa kuwa darasani?
Aliwajibu kuwa hataki tena shule, ameamua kwenda Dar es Salaam kutafuta maisha.
Wanamuziki hao walitumia busara wakamkalishi chini na kumsihi alale pale klabuni. Madhumuni yao ni kwamba waltaka Mabraka aweze kufikiria kwa utulivu juu ya uamuzi yake ya kuacha shule.
Kesho yake wanamuziki hao walishikwa na bumbuwazi baada ya kumkuta Mbaraka akifanya mazoezi ya kupiga gitaa. Kabla ya hapo walimfahamu kuwa yeye ni mpulizaji wa filimbi.
Kwa kuwa walikuwa na shida ya mpiga gitaa la rhythm, walimshauri aache safari ya kwenda Dar es Salaam, abaki kwenye bendi yao kama mpiga gitaa hilo naye alikubali.
Mbaraka alijikuta amekubaliwa kujiunga katika bendi hiyo pasipo kutarajia.
Wakati huo ni wapiga tarumbeta, saxophone na gitaa la solo pekee ndio waliokuwa wakilipwa mshahara kwa mwezi.Wengine wote walikuwa wakipata posho kidogo kila lilipopigwa dansi.
Siku moja wanamuziki wa bendi hiyo ya Morogoro Jazz walialikwa kwenda Dar es Salaam kwa ajili ya mashindano kati yao dhidi ya bendi ya Kilwa Jazz.Kabla ya kuondoka Mwinshehe ‘alitikisa kiberiti’ kwa kugoma kwenda Dar es Salaam kwa kuwa alikuwa halipwi chochote.
Kwa mara nyingine tena busara na hekima za viongozi wa bendi hiyo zilitumika, wakakubali kumlipa mshahara wa shilingi 120 kwa mwezi.
Mpiga solo ambaye aliyekuwa akilipwa shilingi 150, naye akatunisha misuri kwa kugoma kwenda Dar es Salaam kwa hoja kwamba mpiga rhythm hastahili kupata mshahara.
Mbaraka akawatoa hofu viongozi hao juu ya mgomo wa mpiga solo huyo, akasema kuwa yeye ataweza kupiga pia gitaa hilo.
Bendi ya Morogoro Jazz ikaenda Dar es Salaam huku ikiwa imejawa na tashwishiwi juu ya ushindani uliokuwa ukiwakabili kati yao na bendi ya Kilwa Jazz.
Wakati huo bendi ya Kilwa Jazz ilikuwa tishio ukizingatia wanamzuki wakubwa waliokuwepo katika bendi hiyo akina Ahmed Kipande, Kassimu Mapili, Juma Mrisho ‘Ngulimba wa Ngulimba’ na Duncan Njilima.
Viongozi hao wa Morogoro Jazz wakamkabidhi gitaa la solo Mbaraka Mwinshehe Mwaruka, naye bila ajizi siku hiyo ‘Nyota ya Jaha’ ilimuangazia upande wake.
Alilicharaza gitaa hilo kwa umahiri mkubwa katika nyimbo zote zilizokuwa zimepangwa, hadi mwisho wa mashindano bendi yao ikaibuka kidedea kwa ushindi.
Baada ya tukio hilo ambalo halikutegemewa na wengi, Mbaraka Mwinshehe akapandishiwa mshahara hadi ukafikia shilingi 250 kwa mwezi, ambazo zilikuwa ni kiwango cha juu sana miaka hiyo.
Mwinshehe alikuwa na kipaji cha ziada ambacho wanamuziki wengi wamekosa. Alikuwa na uwezo wa kuimba huku akilikung’uta gitaa la solo.
Aliwahi kutunga, kuimba na kushiriki kikamilifu kupiga gitaa la solo nyimbo nyingi za bendi hiyo. Baadhi ya nyimbo hizo ni kama Shida, Nateseka, Safari siyo kifo, Dina uliapa, Maudhi, Penzi la mashaka, Heshima kwa Vijana , Harusi imevunjika , Mshenga No.1 na Nisalimie Zaire.
Wimbo huo Nisalimie Zaire aliutunga kwa ajili ya kumuaga rafiki yake mpigaji gita la rhythm na kuimba sauti ya pili, Koko Malalii aliyekuwa raia wa kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), ambaye alikuwa akipiga gitaa katika bendi hiyo.
Walikuwa marafiki ‘walioshibana’ sana na mara alipoondoka, ndipo akamtungia wimbo huo. Nyimbo zingine zilikuwa Baba mdogo, Mwese, Kibena, Naogopa utanisumbua, Ni siku nyingi, Regina, Kwa ajili yako na Dr. Kreluu.
Wimbo huo aliutunga mahsusi kwa ajili aliyekuwa mkuu wa mkoa Iringa wakati huo, Dk. Kreluu aliyeuawa na mkulima aliyejulikana kwa jina la Mwamwindi, ambaye baadae yaelezwa kuwa alihukumiwa kunyongwa hadi kufa.
Nyimbo zingine alizotoka nazo Mbaraka ni za Harusi imevunjika, Mapenzi shuleni na Sembuli. Wimbo huo wa Sembuli ulikuwa wa maombolezo ya kifo cha marehemu Gibson Sembuli, aliyekuwa mzaliwa wa Morogoro na mcheza kandanda katika mkoa huo baadaye alijiunga na klabu ya Yanga ya Dar es Salaam na timu ya Taifa.
Zingine ni za Matilda, Nalilia raha, Nikupendeje, Mapenzi yanitesa Jogoo la Shamba na nyingine nyingi.Mfano mwingine ni pale alipotunga wimbo ukiwa ni ‘kijembe’ mahsusi kwa hasimu wake mkubwa kimuziki, Juma Kilaza aliyekuwa akiongoza bendi ya Cuban Marimba.
Bendi ya Morogoro Jazz alikuwa na wanamuziki mahiri ambao waliifikisha katika mafanikio hayo. Kwa uchache nakutajia majina ya baadhi yao.
Walikuwa ni akina Mzee Seif Ali, Tosi Malekela, Suli Bonzo, Kilongola, Lazaro Bonzo na Mpalanje. Wengine walikuwa Kazingoma, Simaro Kasansa, Kasinde, Matata, Zanda Ngokoko, Athumani na Paschal.
Kipindi hicho Wapenzi wa muziki waliweza kuondoka Dar es Salaam kwenda mjini Morogoro kuvinjari siku za mwisho wa wiki, katika bendi ya Cuban Marimba au Morogoro Jazz.
Baadaye mwaka 1973 Mbaraka Mwinshehe alijitoa toka katika bendi ya Morogoro Jazz, iliyokuwa ikipiga katika mitindo ya Masika, Likembe, Zolelanga, Sululu na Mahoka.
Akaunda bendi ya Super Volcano akisaidiana na Charels Kasembe, yeye akaendelea kuwa kiongozi wa bendi hiyo hadi mauti yake yalipomfika.
Nguli huyu alikumbwa na mauti baada ya kupata ajali ya gari iliyoyafupisha maisha ya mwanamuziki huyo Januari 12, 1979.
Kwa mujibu wa shuhuda wa ajali hiyo aliyejulikana kwa majina ya Zebedee Japhet Kinoka, maarufu kama Super Zex, alieleza kuwa kifo cha Mbaraka Mwinshehe kilitokea majira ya saa 7 mchana Januari 12, 1979 alipokuwa anatoka maeneo ya Kisauni, jirani na mji wa Mombasa.
Alisema kuwa mwanamuziki huyo alikuwa ameenda kumtembelea mtanzania mwenzake aliyekuwa akimiliki hoteli huko.
Kinoka alisema alipofika karibu na kanisa la Kongoya, aliliona gari aina ya Peugot 404, lenye rangi nyeupe likitoka upande wa Bush bar. Gari hilo lilikuwa katika mwendo mkali likaligonga roli moja lililokuwa likitokea upande mwingine. Watu walokuwa karibu wakakimbilia kungalia ajali akiwemo yeye.
Mara moja akamtambua Mbaraka na kuwambia watu kuwa huyo ni mwanamuziki Mtanzania anaitwa Mbaraka Mwinshehe.Iliwalazimu kuanza kukata mabati ili kumuondoa Mbaraka aliyekuwa amebanwa miguu katika gari lile akiwa bado yu hai.
Wakati kazi hiyo inaendelea Zebedee alikimbilia kwenye baa ya Kengeleni, ambako bendi ya Jamhuri Jazz ya Tanga ilkuwa ikitoa burudani ya muziki. Akawambia kuwa mwenzao kaumia sana, nao wakatoka mbio kwenda kushuhudia.
Walifanikiwa kumtoa Mbaraka kwenye gari hilo, akakimbizwa hadi katika hospitali ya Makadara, mjini Mombasa.Zebedee pia akatumwa kuwafuata wanamuziki wa bendi ya Super Volcano ambao wakati huo walikuwa wameanza kupiga muziki wa mwanzo wakimsubiri Mbaraka katika ukumbi wa baa ya Zambia.
Wanamuziki walipofika hospitalini hapo, wakaambiwa watoe damu ya kumuongezea kiongozi wao Mabaraka Mwinshehe.Kila mmoja akaanza kukwepa kutoa damu kwa visingizio mbalimbali. Baada ya muda mchache Mbaraka Mwinshehe akafariki dunia akiwa na umri mdogo wa miaka 34 tu!.
Mwili wa Mbaraka akasafirishwa hadi mpakani mwa Tanzania na Kenya ukapokewa na ndugu, jamaa, marafiki na maofisa wa Wizara ya Utamaduni.
Baadae mwili wa Mbaraka Mwinshehe akazikwa katika nyumba yake ya milele kijijini kwake Mzenga Wilayani Kisarawe, mkoa wa Pwani.
Mwaka huu umetimia mwaka wa 40 tangu Mbaraka Mwinshehe Mwaruka kufariki dunia, tungo za nyimbo na sifa za kazi zake zitaendelea kudumu vizazi kwa vizazi.
Nyimbo nyingi za bendi ya Morogoro Jazz na Super Volcano bado zinapendwa na kurindima kwenye baadhi ya vituo vya redio na sehemu zingine za burudani hadi leo.
Binti yake Taji Mwaruka, ndiye aliyefuata nyayo za baba yake, ambapo alikuwa akiimba na kuliungurumisha gitaa zito la besi katika bendi ya marehemu baba yake ya Super Volcano. Taji kwa taarifa za hivi karibuni zimeeleza kuwa ameachana na mambo ya muziki, ameamua kuwa mfanyabiashara huko Aghaibuni.
Mungu aipumizishe roho yake pahala pema peponi, Amina.
Mwisho.
Mwandishi wa makala hii anapatikana kwa namba: 08713331200, 0767331200 na 0784331200.
Hivyo makala MBARAKA MWINSHEHE UKOSEFU WA DAMU KUONGEZEWA KULISABABISHA KIFO CHAKE.
yaani makala yote MBARAKA MWINSHEHE UKOSEFU WA DAMU KUONGEZEWA KULISABABISHA KIFO CHAKE. Wakati huu, pengine unaweza kutoa faida na wewe wote. Sawa, kuona katika post nyingine makala.
Wewe ni sasa kusoma makala MBARAKA MWINSHEHE UKOSEFU WA DAMU KUONGEZEWA KULISABABISHA KIFO CHAKE. mahali kiungo https://somalatest.blogspot.com/2019/03/mbaraka-mwinshehe-ukosefu-wa-damu.html
0 Response to "MBARAKA MWINSHEHE UKOSEFU WA DAMU KUONGEZEWA KULISABABISHA KIFO CHAKE."
Post a Comment