Loading...

BENDI YA MAQUIS ILIYOTIKISA ANGA YA MUZIKI

Loading...
BENDI YA MAQUIS ILIYOTIKISA ANGA YA MUZIKI - Hallo rafiki SOMA LATEST, Katika makala kusoma wakati huu na kichwa BENDI YA MAQUIS ILIYOTIKISA ANGA YA MUZIKI, tumeandaa vizuri kwa makala hii kusoma na kupakua maelezo humo. pengine kujaza posts makala afya, makala general, makala kisiasa, makala kitamaduni, makala kiuchumi, makala mambo mapya, makala michezo, sisi kuandika anaweza kuelewa. Naam, furaha ya kusoma.

title : BENDI YA MAQUIS ILIYOTIKISA ANGA YA MUZIKI
link : BENDI YA MAQUIS ILIYOTIKISA ANGA YA MUZIKI

soma pia


BENDI YA MAQUIS ILIYOTIKISA ANGA YA MUZIKI

Na Moshy Kiyungi,TABORA

Miaka ya 1970 baadhi bendi toka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo(DRC) zilivamia soko la muziki humu nchini zikiporomosha muziki.

Ikumbukwe mwaka 1973, Franco Luambo Luanzo Makiadi akiwa na bendi yake ya T.P. OK. Jazz alikuja hapa nchini na akafanya onyesho kamambe katika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Mwaka mmoja baadae wa 1972 bendi ya Maquis du Zaire, nayo ikaingia kwa mbwembwe na kuweka makazi yake ya kudumu katika jiji la Dar es Salaam.
Makala hii inaizungumzia bendi hiyo ambayo ‘iliwatesa’ baadhi ya Watanzania wapenda muziki wa dansi kwa kuwaporomoshea burudani ya muziki katika kumbi mbalimbali hapa nchini. 

Bendi hiyo ni Maquis du Zaire, iliyotokea Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, ikafia humu nchini miaka 1990.Ili kuipata historia kamili ya bendi hiyo mwaka 1981, nilifanikiwa kufanya mahojiano maalum na mmoja wa waliokuwa viongozi wa bendi hiyo Chimbwiza Mbangu ‘Nguza Vicking’.

Alisimulia kwa kina wasifu wa bendi hiyo akisema kwamba mwaka 1960, vijana wa wakati huo katika mji wa Kamina huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), waliungana na kuunda bendi yao wakaiita Super Theo.


Nguza alisema kuwa bendi hiyo ilikuwa ikitoa burudani tosha kwa wapenzi wa muziki wa mji huo wa Kamina na vitongoji vinavyouzunguka mji huo.Alisema baadae wakaibadilisha majina ya bendi ikawa Super Gabby. Lakini uongozi wa Super Gabby ulitaka kuleta mageuzi katika muziko, mwaka 1972, wakabadilisha majina rasmi kuwa Maquis du Zaire.

Mwaka huohuo bendi hiyo iliingia hapa Tanzania wakapitia nchini Uganda.
Walipofika katika jiji la Dar es Salaam walipata mkataba wa kupiga muziki katika ukumbi wa Mikumi Tours, uliokuwa maeneo la Tazara Buguruni jijini Dar es Salaam.

Baada ya kumaliza mkataba wao waliondoka wakaenda kupiga muziki katika Klabu ya Hunters kwa kipindi kifupi.

Kisha viongozi wa bendi hiyo wakafanya mazungumzo na mfanyabiashara Hugo Kisima, aliyekuwa akimiliki wa ukumbi wa Safari Resort maeneo ya Kimara, jijini Dar es Salaam. Wakaanza kupiga muziki kwa mkataba na mfanyabiashara huyo.

Februari 1977 viongozi wa bendi hiyo ya Maquis du Zaire, waliamua kukiongezea nguvu kikosi chao. Hivyo walimtuma Tchibangu Katayi ‘Mzee Paul’ aliyekuwa mwanamuziki wa bendi ya Maquis du Zaire. Pia alikuwa mmoja kati ya viongozi wa bendi hiyo.Mzee Paul aliwachukua baadhi ya wanamuziki ili kuja Tanzania kuongeza nguvu katika bendi ya Maquis du Zaire.

‘Mzee Paul’ alibahatika kuwachukuwa wanamuziki akina Kikumbi Mwanza Mpango ‘King Kiki’, mtunzi na mwimbaji, Kanku Kelly kwa upande wa tarumbeta., Ilunga Banza ‘Mchafu’, aliyekuwa akiungurumisha gitaa la besi, Mutombo Sozy aliyekuwa akizicharanga drums, na mnenguaji Ngalula Tshiandanda.

Wakati huo Maquis du Zaire walikuwa wakicheza muziki wakitumia mtindo wa ‘Chakula Kapombe’, ambao kwa Watanzania ulikuwa mpya na ukapendwa mno na mashabiki.

Kufika kwa wanamuziki hao kulileta changamoto kubwa katika muziki. Tungo nzuri za Kikumbi Mwanza Mpango ‘King Kiki’, zilikuwa chachu masikioni mwa wapenzi wa muziki wa dansi. Kiki pia yaelezwa kuwa ndiye aliyeleta Mapinduzi makubwa ya muziki hapa nchini Tanzania.

Maquis du Zaire wakaazisha mtindo mwingine wa ‘Kamanyola’ uliowapagaisha wapenzi na wadau toka pembe zote za jiji la Dar es Salaam.

Mwishoni mwa 1977, Marquis du Zaire, walimaliza mkataba kwa Hugo Kisima, wakaondoka.Bahati nyingine ikawadondokea tena baada kuingia mkataba mwingine wa kupiga muziki kwa mzee Makao, aliyekuwa akimiliki ukumbi wa Savannah, maeneo ya Ubungo.Wakiwa Savannah, walianzisha mitindo ya ‘Sanifu’ na ‘Ogelea piga mbizi’.

Lakini ukumbi huo ukabadilishwa jina ukaitwa White House. Ikumbukwe kwamba Maquis pia ilikuwa ikipiga kwenye ukumbi wa Mpakani, maeneo ya Mwenge.Mwishoni mwaka Maquis du Zaire 1978 waliamua kuimarisha tena kikosi chao kwa kuwaleta wanamuziki wengine wapya kutoka DRC.Iliwaleta akina Kabeya Badu, Kalala Mbwebwe, Ngoyi Mubenga na Khatibu Iteyi Iteyi.

Bendi hiyo ilikuwa ikiongozwa na wanahisa akina Chinyama Chiyaza ‘Chichi’, Chibangu Katayi ‘Mzee Paul’, Chimbwiza Mbangu Nguza ‘Nguza Vicking’, Mutombo Lufungula ‘Audax’ na Mbuya Makonga ‘Adios’.

Chini ya uongozi huo, miaka ya 1980 mafanikio makubwa yalionekana, mojawapo ni lile la kuanzisha Kampuni iliyofahamika kama Orchestra Maquis Company (OMACO).

Kampuni hiyo iliweza kumiliki shamba la matunda, wakalima kwa kutumia treka zao maeneo ya Mbezi nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam.Mazao yao walikuwa wakiyapeleka na kuuza katika Soko Kuu la Kariakoo jijini Dar es Salaam.OMACO pia ilimiliki mradi mwingine wa viwanja tisa na nyumba kadhaa, maeneo ya Sinza, jijini Dar es Salaam.

Aidha iliwahi kuingia mkataba wa kuitangaza kampuni ya magari makubwa ya SCANIA.Vijana wa wakati huo watakumbuka jinsi ukumbi wa White House ulivyokuwa ukifurika watu kila siku za Jumamosi.Waliwashuhudia wanamuziki wa bendi hiyo waliokuwa watanashati, nidhamu ya hali ya juu hususan wakiwa jukwaani wakifanya vitu vyao.

Enzi hizo ilikuwa ukiingia katika ukumbi huo wa White House, mbele yako macho lazima yakutane na mbao zilizokomelewa juu ya mwembe uliokuwa ukumbini hapo, zikiwa zimenakshiwa kwa maandishi ya majina ya wanamuziki wote.

Maquis du Zaire ambayo ilikuwa ikipiga muziki mara moja kwa wiki, ilikuwa ikifika usiku wa manane, wanasisitisha muziki kwa muda na kusikika kipaza sauti kikiuliza “Wapenzi mumekuja na miswakii? Wapenzi walikuwa wakijibu “ndiyooo…” Wanaelezwa dawa ya meno ipo hapo.

Watu wengi hawakuwa na haja ya kuchukua teksi kurudi nyumbani kwani muziki wa Maquis du Zaire, ulikuwa unarindima hadi alfajiri. Muda ambao mabasi ya UDA ya Ikarus yalikuwa yameanza kazi. Wakati huo hazikuwepo ‘Dala dala’, Bajaji wala Pikipiki.

Kupitia ubunifu waliokuwa nao wanamuziki hao waliweza kubadilisha mitindo mbalimbali kwa nyakati tofauti. Mitindo hiyo ilikuwa ya ‘Chakula kapombe’, ‘Kamanyola’, ‘Sanifu’, ‘Bishe Bishe’, ‘Zembwela’, ‘Chekecha’ na Ogelea Piga mbizi.

Mpulizaji wa Tarumbeta Mwema Mudjanga ‘Mzee Chekecha’ alikuwa akiwahamasisha wapenzi wake ukumbini humo akitoa

Alikuwa Mwema Mudjanga ‘Mzee Chekecha’ aliyekuwa akinogesha zaidi mitindo hiyo ukumbini. Licha ya kazi yake ya kupuliza tarumbeta, aliweza kuwainua vitini wapenzi kwenda kucheza, akitumia vibwagizo vya “Chekeee…. Chekechaaa” “Cheza Kamanyola bila jasho…”, “Tusangalaa”, “Aima imaa”, ‘Bishe bishee”, “Saa… Sanifuu”, “cheza Kamanyolaa” “cheza kwa maringo”, “ Cheza ukijidai” na mengine mengi.


Maquis du Zaire wakati huo ilikuwa imesheheni wanamuziki takriban 40, wenye talanta zinazopishana.Kwa idadi hiyo, laiti kama wangelikuwa na tamaa, wangeliweza kupiga muziki katika kumbi tatu tofauti kwa wakati mmoja.Mpendwa msomaji naomba nikujuze au kukumbusha kikosi kamili kilichokuwa kinatengeneza bendi hiyo kwa nyakati tofauti.

Safu ya waimbaji walikuwepo akina Kikumbi Mwanza Mpango ‘King Kiki’, Mbuya Makonga ‘Adios’, Mutombo Lufungula ‘Audax’, Mukumbule Lolembo ‘Parashi’, Kabeya Badu, Kalala Mbwebwe, mapacha Kassalo Kyanga na Kyanga Songa.

Wengine walikuwa Kiniki Kieto, Abubakar Kasongo Mpinda ‘Clayton’, Mbombo wa Mbomboka, Tshimanga Kalala Assosa, Masiya Radi ‘Dibakuba kuba’, Issa Nundu na waimbaji wa kike Tabia Mwanjelwa, Rahma Shaari na Anna Mwaole.

Wapiga gitaa la solo alikuwepo Chimbwiza Nguza Mbangu ‘Nguza Vicking’, ambaye kwa umahiri wake wa kulicharanza gita hilo, wapenzi walimpachika cheo cha juu kabisa jeshini cha ‘Field Marshal’.Wengine katika gitaa hilo walikuwa akina Ilunga Lubaba, Dekula Kahanga ‘Vumbi’, na Mbwana Suleiman ‘Mbwana Cox’.

Gitaa la rhythm walikuwepo Mulenga Kalonji ‘Vata’, Omari Makuka na Steven Kaingilila Mauffi. Halikadharika walikuwepo akina Mbambu Kazadi, Mondo Mondonde na Nawayi Kabwila.

Kwa upande wa uungurumishaji wa gitaa zito la besi walikuwa akina Ilunga Banza ‘Banza Mchafu’ ambaye aliyejizolea umaarufu mkubwa kwa kulimudu gitaa hilo akiwa kajitwisha kwenye upara uliozungushiwa simbi kichwani kwake. Wengine walikuwa Ibrahimu na Mujos wa Bayeke.

Kwa upande wa wapuliza Saxophone ‘mdomo ya bata’ walikuwepo akina Mafumu Bilali ‘Bombenga’ au‘Super Sax’, Khatibu Iteyi Iteyi, Kalamzoo, Alex Kanyimbo, Akulyake Suleimani ‘King Mallu’, Roy Mukuna ‘Mukuna wa Mukuna’, Chibangu Katayi , Comson Mkomwa na Majengo Selemani.

Wapulizaji tarumbeta walikuwepo akina Mwema Mudjanga ‘Mzee Chekecha’ Nkashama Kanku Kelly, Mioma wa Mwamba ‘Mzee Tito’, Kayembe Ndalabuu ‘Trumbloo’, Mpoyo Kalenga, Berry Kankonde, Kaumba Kalemba, Ngoi Mubenga, Ilunga Ngoi ‘Bizos’, Morgan Machege na Ngenda Kalonga.

Pamoja na uimbaji Mbuya Makonga ‘Adios’ alikuwa anabofya kinada, huku Mutombo Sozzy akizicharaza drums akisaidiana na Matei Joseph.

Tumba zilikuwa zikigongwa na Siddy Morris ‘Super Konga’ na Pulukulu Wabandoki Motto.Kwa upande wa wanenguaji walikuwa akina ‘Washa Washa’, Dulla ‘Panga Panga’, Wandema Rashid, Anna Mganga, Kinacho, Mwajuma, Frida Shirima, Zuwena na Ngalula Tshiandanda, wakiongozwa na Nkulu Wabangoi.

Ikiwa katika ukumbi huo wa White House, bendi hiyo ilitoka na vibao vingi vikiwemo vya Double double, Clara, Kyembe, Maiga, Mpenzi Luta, Ngalula, Nasononeka, Nimepigwa ngwala, Promotion, Ngalula, Karubandika na Noelle Bonane. Wimbo huo ulikuwa ukipigwa mahsusi nyakati za Krimasi na mwaka mpya.

Zingine zilikuwa Dora mtoto wa Dodoma, Balimwacha, Malokelee, Promotion, Seya, Sophia, Sumu ya mapenzi, Sababu ya nini, Zowa, Uba, Safari ya Mbeya, Wakati nikiwa mdogo na nyingine nyingi zisizo idadi.

Kuna msemo usemao “Cha kuazima hakistiri maungo” msemo huo uliisibu bendi ya Maquis du Zaire baada ya kutokea sintofahamu kati ya mmiliki wa ukumbi na uongozi wa bendi. Hatma yake Maquis du Zaire ikasambaratika, wakaacha ukumbi huo uliokuwa jirani na kona ya kwenda Msewe, ukabadilishwa kuwa gereji hadi leo.

Baadhi ya wanamuziki hao walijikusanya na kuisuka upya bendi hiyo, kwa jina jingine la Maquis Original.Ikaanza kupiga muziki katika kumbi za Wapiwapi’s uliopo Maduka mawili, Chang’ombe na CCM Kata ya 14 Temeke.
Baadae wakahamia ukumbi mpya kwa wakati huo wa Lang’ata, Kinondoni walipopafanya kuwa makao yao makuu.

Baadhi ya wanamuziki hao ni pamoja na Mutombo Lufungula ‘Audax’, Tshimanga Kalala Asossa, Dekula Kahanga ‘Vumbi’, Mukumbule Lolembo ‘Parashi’, Mukuna Roy, Ilunga Banza ‘Mchafu’, Mujos wa Bayeke, Kaumba Kalemba, Mulenga Kalondji ‘Vata’ na wengine wengi.

Maquis Original iliongeza nguvu zaidi kwa kuwaleta wanamuziki wengine toka DRC, muda mfupi kabla ya kuondoka mpiga gitaa la solo, Dekula Kahanga ‘Vumbi’ kwenda Stockholm nchini Sweden.

Wanamuziki hao walikuwa Kivugutu Moto na Chatcho, aliyekuwa akilicharaza gitaa la solo, waimbaji Freditto Butamu na Luhembwe Mwahitwa ‘Bobo Sukari’.

Safu hiyo ya Maquis Original ilitikisa wapenzi na mashabiki wake katika ukumbi wa Lang’ata kwa nyimbo zao kali za Mangolibo, Mayanga, Makumbele na nyingine nyingi.Wimbo wa Ngalula ulikuwa ukitia fora mbapo wakati wa ‘chorus’, Tshimanga Assosa, alikuwa akimpandisha mori mpiga gita la solo Dekula Kahanga ‘Vumbi’ akimwita “vumbiii… Vimbiiii… Vumbiii…”

Nyimbo za Maquis Original ziliweza kukonga nyoyo za wapenzi wao kwa mitindo waliyobuni hapo ya ‘Washawasha’ na ‘Sendema’.Aidha Maquis Original walikuwa shabiki wao mkubwa aliyejulikana kwa jina la ‘Magoma moto’. Alikuwa akiachiwa uwanja akionesha uhodari wake wa kucheza mtindo hiyo, huku akiwa kajitwisha chupa yenye bia kichwani chake.

Waswahili wanasema kuwa “ Lakuvunda halina Ubani” Maquis Original nayo ikaondoka katika medani ya muziki, ni zaidi ya miaka 27 sasa toka jina la Maquis Original,liliposambaratika katika miaka ya 1990.
Mwanamuziki mahiri Tshimanaga Kalala Assosa ‘mtoto mzuri’, alijitoa Kimasomaso kwa kutumia weledi wake, akalienzi jina la Maquis.

Alianzaisha bendi ya ‘Bana Maquis’ ambayo hupiga na kukumbushia nyimbo zilizopigwa na Maquis du Zaire, Maquis Original na za kwao.Mpenzi msomaji kwa mapenzi yake Mungu, idadi kubwa miongoni mwa wanamuziki wanaotajwa katika makala hii, wameshatangulia mbele zake.

Wengine wanaumwa maradhi mbalimbali akiwemo Mbombo wa Mbomboka.
Mungu aziweke roho zao pahala pema peponi waliotangulia mbele zake na awape tahfifu wanaoumwa, amina.



Hivyo makala BENDI YA MAQUIS ILIYOTIKISA ANGA YA MUZIKI

yaani makala yote BENDI YA MAQUIS ILIYOTIKISA ANGA YA MUZIKI Wakati huu, pengine unaweza kutoa faida na wewe wote. Sawa, kuona katika post nyingine makala.

Wewe ni sasa kusoma makala BENDI YA MAQUIS ILIYOTIKISA ANGA YA MUZIKI mahali kiungo https://somalatest.blogspot.com/2019/03/bendi-ya-maquis-iliyotikisa-anga-ya.html

Subscribe to receive free email updates:

0 Response to "BENDI YA MAQUIS ILIYOTIKISA ANGA YA MUZIKI"

Post a Comment

Loading...